Falme za Kiarabu na Sudan kuwasaidia waasi wa Libya

0
694

Ujumbe wa maafisa kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umekutana na maafisa wa Serikali ya Sudan kujadili mpango wa kumsaidia mbabe wa kivita anayeendesha mapambano ya kuiondoa madarakani serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Maifa nchini Libya, Jenerali Khalifa Haftar.

Ujumbe huo ambao ulikuwepo nchini Sudan umejadili masuala mbalimbali ikiwemo mpango wa kutafuta wapiganaji ambao watamsaidia Jenerali Haftar katika mapigano yake.

Mapema mwezi Januari mwaka huu Serikali ya Sudan imeahidi kuchunguza tuhuma za kuwepo kwa raia wa nchi hiyo wanaofanya kazi za ulinzi katika vituo vya mafuta vinavyomilikiwa na kampuni moja kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mgogoro wa Libya umechukua sura mpya baada ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu (Human Rights Watch) kutoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu shambulio lililofanywa na ndege zisizo na rubani za UAE. Shambulio hilo lililolenga kituo kimoja cha afya karibu na Mji Mkuu wa Libya, Tripoli Novemba mwaka jana lilisababisha vifo vya watu nane huku wengine 27 wakijeruhiwa.

Wakati hayo yakiendelea Uturuki imemshutumu Jenerali Haftar kwa kutaka kuanzisha utawala wa kidikiteta katika eneo la Mashariki mwa Libya huku ikiapa kuendelea kuisaidia serikali halali.

Aidha, jenerali huyo ametangaza kusitisha mapigano dhidi ya serikali ili kupisha wananchi wafunge katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Wakati huo huo Shirika la Kutetea Haki za Binadamu (Amnesty Internatinal) limetoa ushahidi unaoonesha kukiukwa kwa vikwazo vya silaha ambavyo Umoja wa Mataifa (UN) uliiwekea Sudan Kusini.