Waziri wa Afya visiwani Zanzibar, Hamad Rashid ametangaza ongezeko la wagonjwa wapya saba wenye maambukizi ya virusi vya corona.
Ongezeko hilo linafanya idadi ya waathirika wa homa ya mapafu (COVID-19) visiwani humo kufikia 105 kutoka 98 waliotolewa taarifa Aprili 24 mwaka huu.
Waziri Rashid amesema kuwa wagonjwa wote wapya ni raia wa Tanzania.
Wakati huo huo, wagonjwa 36 wameruhusiwa kurejea makwao baada ya vipimo kuonesha kuwa hawana dalili za ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kikohozi, mwili kuchoka, kifua kubana, na maumivu ya kichwa.
Hata hivyo wote walioruhusiwa kurejea nyumbani wameshauriwa kubaki kwenye nyumba zao kwa siku 14 huku afya zao zikiendelea kuchunguzwa kabla ya kuruhusiwa kurejea kwenye shughuli zao.
Wizara hiyo imewasihi wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo, pamoja na kutoa taarifa pindi wanapohisi kuwa wagonjwa.