Bei elekezi ya sukari kwa mikoa yote

0
1721

Wakati sakata la bei ya sukari likiendea kushika kasi nchini, serikali imesema kuwa haitokubali kuona wananchi walio wengi wanaumia kwa ajili ya manufaa ya watu wachache.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alipokuwa akizungumza katika kikao cha pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa ambao kwa pamoja waleeleza kuwa hakuna uhaba wa sukari nchini.

Waziri Hasunga amesema kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamepandisha bei ya bidhaa hiyo kiholela wakitoa visingizio vya uhaba wa bidhaa hiyo kutokana na baadhi ya viwanda kushindwa kuzalisha sukari, na uwepo wa mlipuko wa virusi vya corona, na kwamba wapo wafanyabiashara walioficha sukari kwenye maghala.

Kutokana na wananchi kulia na gharama kubwa ya bidhaa hiyo muhimu, waziri wa kilimo ametangaza bei ya juu ya ukomo kwa mamlaka anayopewa na Sheria ya Sukari Na.26 ya Mwaka 2001 chini ya kifungu cha 11(a).

Hasunga amesema uuzaji wa kilo moja ya sukari kwa shilingi 4,000 au 4,500 kama ilivyo sasa katika baadhi ya maeneo haukubaliki.

“Tunatarajia katika Mkoa wa Dar es Salaam, bei ya ukomo isizidi shilingi 2,600, lakini kwa mkoa uliopo mbali sana, Katavi, bei ya ukomo ni 3,200,” amesisitiza Hasunga.

Hapa chini ni bei ya ukomo wa juu katika mikoa 26 ya Tanzania Bara:

Iringa = 2,900
Mbeya = 3,000
Rukwa = 3,200
Katavi = 3,200
Ruvuma = 3,200
Njombe = 2,900
Lindi = 2,800
Mtwara = 2,800
Arusha = 2,700
Kilimanjaro = 2,700
Manyara = 2,700
Tanga = 2,700
Dar es Salaam = 2,600
Pwani = 2,700
Morogoro = 2,700
Kagera = 3,000
Mwanza = 2,900
Simiyu = 2,900
Shinyanga = 2,900
Geita = 2,900
Mara = 3,000
Kigoma = 3,200
Singida = 2,900
Tabora = 2,900
Dodoma = 2,900
Songwe = 3,000