Ubalozi wa Ufaransa kusaidiana na serikali kupambana na COVID-19

0
635

Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania ameelekeza sehemu ya mamilioni yaliyotolewa na nchi hiyo kwa serikali kwa ajili ya kupambana na mlipuko wa virusi vya Corona nchini Tanzania.

Balozi Frédéric Clavier amesema kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, Ufaransa imeipa Tanzania kiasi cha Euro milioni 310 (shilingi bilioni 777.9) kwa ajili ya afya, maji na usafi wa mazingira.

Hivi sasa ubalozi huo unaangazia kuelekeza Euro 500,000, (shilingi bilioni 1.3) katika mapambano dhidi ya homa ya mapafu (COVID-19), kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa afya na vifaa vya matibabu.

Kwa kushirikiana na makampuni binafsi nchini kama SAT na TOAM Ubalozi wa Ufaransa utaelekeza Euro 500,000 (shilingi bilioni 1.3) katika chakula, msaada wa kiuchumi na kinga za Corona kwa wananchi wa vijijini kwani wapo kwenye hatari kubwa zaidi endapo watapata maradhi hayo.

Clavier, amesema atahakikisha Tanzania inafaidika na misaada kutoka nchi zenye mahusiano na Ufaransa kulingana na idadi yake ya watu.

Aidha, balozi huyo ameyataka makampuni yote ya kifaransa nchini kuhakikisha yanasaidia kutoa vifaa tiba na vifaa vya usafi kwa serikali ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Mnamo Aprili 18, Rais Emmanual Macron wa Ufaransa alitangaza kuelekezwa kwa Euro bilioni 1.2 (shilingi trilioni 3.01) katika kupambana na COVID-19 barani Afrika.