Ebola yaendelea kusababisha vifo DRC

0
2125

Maafisa wa afya katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wamethibitisha kuwa watu 24 wamefariki dunia katika kipindi cha wiki moja iliyopita baada ya kuugua ugonjwa wa Ebola kwenye eneo la mashariki la Jamhuri hiyo.

Kufuatia hali hiyo, maafisa hao wa afya wametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo la Mashariki kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huo hatari.

Maafisa hao wa afya katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wamesema kuwa juhudi za kuwahudumia wagonjwa wa Ebola zimekua zikikwamishwa na makundi ya waasi ambayo yamekua yakiendeleza uhalifu katika eneo la mpaka wa Jamhuri hiyo na nchi za Rwanda na Uganda.

Akizungumza hivi karibuni na waandishi wa habari mjini New York nchini Marekani, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ameonya kuwa ghasia zilizozuka hivi karibuni katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zinakwamisha juhudi za kuudhibiti ugonjwa huo wa Ebola.

Katika kikao chake maalum kinachotarajiwa kufanyika hapo kesho Oktoba 17, Shirika la Afya Duniani (WHO) lina mpango wa kutathmini iwapo litangaze mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kama janga la dharura la kiafya linalohitaji uangalizi wa Jumuiya ya Kimataifa .