Takribani watu 18 wamefariki dunia baada ya magari mawili kugongana leo asubuhi katika Kijiji cha Kilimahewa, wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
Ajal hiyo imehusisha basi dogo la abiria (coaster) lililokuwa likitoka Kijiji cha Magawa kwenda jijini Dar es Salaam ambalo limegongana uso kwa uso na lori la mizigo lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya kusini mwa Tanzania.
Kutokana na ajali hiyo Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa watu waliofariki, ambapo amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo kufikisha salamu hizo kwa familia za marehemu, na kwamba anaungana nao katika kipindi hiki cha kuondokewa na wapendwa wao.
“Nawaombea familia za marehemu wote, ndugu, jamaa na marafiki kuwa na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, kuwapoteza Watanzania wenzetu kwa idadi kubwa namna hii inaumiza sana,” amesema Rais Magufuli.
Aidha, amevitaka vyombo vya usalama barabarani kuhakikisha vinachukua hatua madhubuti za kuzuia ajali za barabarani na amewataka madereva na wote wanaotumia barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali ambazo zinagharimu maisha ya watu na uharibifu wa mali.