Serikali imewaagiza viongozi wote wa dini nchini kuchukua tahadhari sana wakati wa ibada ili kuhakikisha wanadhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na viongozi wa dini kuhusu hali ya maambukizi ya virusi vya corona ambapo amesema licha ya kuwa Rais John Magufuli alisema kwamba serikali haitofunga nyumba za ibada, lakini ni jukumu la viongozi kuhakikisha waumini wanakuwa salama.
“Ni jukumu letu sisi kuhakikisha tunafanya ibada kwa njia isiyo hatarishi kwetu na kwa waumini wetu. Wataalamu wanashauri waumini kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu.
“Tunaomba pia ibada ifanyike muda mfupi, pia wekeni utaratibu wa kupunguza msongamano wa waumini wakati wa kuingia na kutoka katika nyumba za ibada,” amesema Ummy
Akizungumzia hali ya maambukizi ya virusi hivyo, Ummy Mwalimu amesema kwamba tayari maambukizi yao yameanza kuenea ndani ya jamii (local transmission), kutoka kuingizwa nchini, na kwamba inapofikia hatua hiyo, itakuwa vigumu kujua mtu alipopata maambukizi.
“Ugonjwa tumeletewa kutoka nje, hivi sasa takwimu za jana, juzi na wiki iliyopita tumeanza kuambukizana wenyewe kwa wenyewe. Ili viongozi wangu wa dini naomba niliweke wazi ‘its no longer imported cases, tumeanza local transmission.’
Aidha, ameongeza kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti ili kudhibiti maambukizi zaidi, na kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa salama, huku pia akiwaasa wananchi kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kuendelea kunawa mikono kwa sabani na maji tiririka, kutumia vitakasa mikono, kuepuka mikusanyiko na safari zisizo za lazima.