Siku ya chakula Duniani yaadhimishwa

0
2135

Tanzania leo inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya Chakula Duniani ambapo kitaifa sherehe hizo zinafanyika katika kijiji cha Chamanangwe wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba.

Siku ya Chakula Duniani ilitokana na kuanzishwa kwa Shirika la Chakula Duniani (FAO) Oktoba 16 mwaka 1945 huko Roma nchini Italia, lengo likiwa ni kusimamia haki ya kupata chakula pamoja na haki ya kila mtu kutokumbwa na njaa.

Katika kufanikisha lengo hilo, nchi tajiri duniani zimekua zikitoa ruzuku kwa wakulima wao na kuwatafutia soko la mazao yao.

Siku ya Chakula Duniani inaadhimishwa huku takwimu zikionyesha kuwa kwa upande wa  nchi zinazoendelea na hasa zilizo kusini mwa jangwa la Sahara Barani Afrika, suala la kutojitosheleza kwa chakula bado ni changamoto kubwa.

Katika kukabiliana na changamoto  hiyo,  kila nchi imeanzisha miongozo, sera, kanuni, sheria na kampeni mbalimbali zenye lengo la kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo.

Kwa upande wa Tanzania, kumekuwa na kampeni katika vipindi mbalimbali ikiwemo ile ya Mapinduzi ya Kijani, Kilimo ni Uti wa Mgongo na Kilimo Kwanza, lengo likiwa ni kujitosheleza kwa chakula na kutumia kilimo kama njia ya kuwainua wakulima kiuchumi na taifa kwa ujumla.

Kauli mbiu ya siku ya chakula duniani kwa mwaka huu ni Juhudi zetu ndio hatma yetu, Dunia bila ya njaa inawezekana ifikapo mwaka 2030.