Kijana mbaroni kwa kufungua ukurasa wa Corona Facebook

0
802

Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limemtia mbaroni Awadhi Luguya (24), mkazi wa Mazimbu, Manispaa ya Morogoro kwa tuhuma za kufungua ukurasa katika mtandao wa kijamii wa Fecebook na kuupatia jina la Coronavirus Tanzania.

Taarifa za Jeshi hilo zinaeleza kuwa, kupitia ukurasa huo, Awadhi alikuwa akisambaza taarifa zisizo rasmi ambazo zimejaa upotoshaji kuhusu ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona (COVID-19).

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema mtuhumiwa alikamatwa Aprili 1, mwaka huu, majira ya saa 11 jioni katika eneo la Mazimbu.

Amesema polisi walipata taarifa kutoka kwa wananchi na kupitia mitandao ya kijamii kuwa kijana huyo amefungua ukurasa huo na anautumia kutoa taarifa ambazo sio rasmi, na zilizojaa upotoshaji mkubwa kwa watu kuhusu Corona.

“Tumemkamata na simu zake zote. Anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani kwa makosa ya matumizi mabaya ya mtandao,” amesema Mutafungwa.