England yapata ushindi wa kwanza ugenini

0
2139

England imepata ushindi wa kwanza ugenini dhidi ya Hispania ndani ya kipindi  cha miaka 31 baada ya kuwabwaga wenyeji wao Hispania kwa mabao matatu kwa mawili kwenye mchezo wa hatua ya makundi katika michuano ya ligi ya mataifa ya Ulaya.

England ndio walikuwa wa kwanza kupata mabao ambapo ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza waliandika mabao hayo matatu na kuwaduwaza wenyeji wa mchezo huo ambao iliwalazimu kusubiri kupindi cha pili kupata mabao yao mawili.

Raheem Sterling wa England amepachika mabao mawili dakika za 16 na 38 huku bao lingine likitiwa kimiani na Marcus Rashford kwenye dakika ya 30 na Francisco Alcacer akifunga katika dakika ya 58 na nahodha wa Hispania, – Sergio Ramos akipachika bao la pili kwa Hispania katika dakika ya 97.

Mara ya mwisho kwa England kupata bao na ushindi wakicheza ugenini dhidi ya Hispania ilikuwa mwaka 1987 ambapo nyota wa England kwa wakati huo Gary Lineker alipofunga mabao yote manne kwenye ushindi wa mabao manne kwa mawili.

Kwa upande wa Hispania,  wenyewe hii ni mara yao ya  kwanza ndani ya kipindi cha miaka 15 kupoteza mchezo wa kimataifa wa kiushindani wakicheza nyumbani  ambapo  walifungwa na Ugiriki mwaka 2003 na kukatisha mfululizo wa michezo 38 bila kipigo.

Mbali na hiyo, hii pia inakuwa mara ya kwanza katika historia ya Hispania kufungwa mabao matatu ama zaidi ndani  kwenye mchezo wa kiushindani wa kimataifa waliocheza nyumbani.