Jiko la mkaa lasababisha vifo vya wanafamilia wanne

0
206

Watu wanne wamefariki dunia katika Kitongoji cha Ngilimba B, Halmashauri ya Ushetu, Shinyanga baada ya kuvuta hewa yenye sumu iliyotokana na mkaa waliouwasha kwenye jiko na kisha kuliweka ndani ya nyumba yao ili kujikinga na baridi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Debora Magiligimba amesema watu hao ni wanafamilia ambapo waligundulika wamefariki baada ya kuvuta hewa hiyo wakiwa wamelala.

Kamanda Magiligimba amewataja waliofariki kuwa ni Masanja Emmanuel (35) ambaye ni baba wa familia hiyo, Mngole Masanja (25) mkewe, Holo Masanja,(05) na Matama Masanja (03) wote wakazi wa Ngilimba.

“Tukio hili limesababishwa na mvua iliyonyesha Machi 27 iliyoambatana na baridi kali ndipo marehemu hao waliamua kulala na jiko la mkaa ndani ya nyumba yao na kusababisha mgandamizo wa hewa kuwa mdogo uliosababisha wavute hewa yenye sumu ya carbon monoxide,”amesema Magiligimba.

Miili ya marehemu hao imekabidhiwa ndugu zao kwa ajili ya taratibu za mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi wa daktari.