Wanaomini rushwa imepungua nchini waongezeka

0
248

Mkurugenzi Mkuu (Mteule) wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Brigedia Jenarali John Mbungo amesema kuwa utafiti uliofanywa kwa mwaka 2018/19 umeonesha kuwa idadi ya Watanzania wanaoamini kuwa vitendo vya rushwa vimepungua imeongezeka kwa asilimia 34.

Akizungumza leo Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma katika hafla ya kumkabidhi Rais John Magufuli ripoti ya utendaji kazi wa TAKUKURU ya mwaka 2018/19 amesema kuwa idadi hiyo imeongezeka kutoka asilimia 37 mwaka 2015 hadi asilimia 71 katika mwaka ulioishia Juni 30, 2019.

Aidha, amesema kuwa ripoti ya Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum – WEF) kwa kushirikiana na sekta binafsi imeonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 28 kati ya nchi 136 kwa ufanisi katika matumizi mazuri ya fedha za umma.

Akizungumzia operesheni za TAKUKURU katika mwaka 2018/19 amesema zimefanikiwa kuokoa shilingi bilioni 82.8 ikilinganishwa na shilingi bilioni 70.3 za mwaka 2017/18 na pia miradi ya maendeleo iliyofuatiliwa imeongezeka kutoka 691 yenye thamani ya shilingi trilioni 1.494 hadi kufikia miradi 1,106 yenye thamani ya shilingi trilioni 1.668.