Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Festo Maduhu, mkazi wa Mtaa wa Benki Kabwe mkoani humo kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake na kisha yeye mwenyewe kujaribu kujiua kwa kisu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema kuwa Machi 22, 2020 majira ya saa tatu asubuhi katika nyumba ya kulala wageni (Negero) mhudumu wa nyumba hiyo, Jesca Michael, mkazi wa Ilolo alikutwa ameuawa kwa kukabwa shingo na kupigwa sehemu za usono na mtuhumiwa huyo.
SACP Matei amesema kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi kwani mtuhumiwa alikuwa anamtuhumu marehemu kuwa alikuwa na uhusiano na mwanaume mwingine ambaye jina limehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi na ufuatiliaji.
Jeshi la polisi lililopokwenda lilimkuta akijichinja koromeo lake kwa kutumia kisu ambapo askari polisi walimuokoa na kumpeleka Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa uchunguzi zaidi wa kitabibu., na mtuhumiwa anaendelea kupatiwa matibabu akiwa chini ya ulinzi na mara apatapo nafuu atahojiwa na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za mauaji na kujaribu kujiua.