Wanamichezo wataka mashindano ya Olimpiki kuahirishwa

0
280

Wanamichezo mbalimbali duniani kote wameomba kuahirishwa kwa mashindano ya olimpiki yaliyopangwa kufanyika mwaka huu kutokana na tatizo la ugonjwa wa Corona uliosamba duniani kote.

Kamati ya Olimpiki Duniani (IOC) imesema haiwezi kufuta mashindano hayo ikiwa imesalia miezi minne kabla ya kufanyika kuanzia Julai 24 hadi Agosti 9, 2020.

Wanamichezo hao wamesema afya ya binadamu ni bora zaidi kuliko mashindano hayo hivyo itakuwa vyema endapo yatasogzwa mbele.

Chama cha mchezo wa riadha cha Marekani kimeomba mashindano ya olimpiki yasogezwe mbele kwa muda wa miezi 12 huku baadhi ya wadau wakiona kufanyika kwa mashindano hayo ni sawa na kuhatarisha maisha ya watu.

Mmoja wa wanamichezo ambaye ameshauri mashindano hayo kutofanyika mwaka huu ni bingwa wa Paralimpiki, Ali Jawad aliyeshinda medali ya shaba kwenye mashindano ya mwaka 2016, Rio de Janeiro nchini Brazil ambapo amesema amewasiliana na maelfu ya wanamichezo wenzake, na wote wanaonelea mashindano hayo yasiwepo kwa mwaka huu.