Wivu wa kimapenzi wasababisha mauaji Bagamoyo

0
290

Jeshi la polisi mkoani Pwani linawashikilia watu watatu wakazi wa Kijiji cha Kibindu wilayani Bagamoyo, kwa tuhuma za kumuua mwanamke mmoja na kisha kumfukia katika shamba la mahindi.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Wankyo Nyigesa amesema kuwa sababu za mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi, ambapo tarehe 10 mwezi huu mume wa mwanamke  huyo aliyefahamika kwa jina Chacha Machagu alimshambulia kwa mapanga, hali iliyosababisha kifo chake.

Amesema baada ya tukio hilo Chacha kwa kushirikiana na wadogo zake wawili walichukua mwili wa mwanamke huyo na kwenda kuufukia katika shamba la mahindi hadi  polisi walipopata taarifa kutoka kwa wasamaria wema na kwenda kuwakamata.

Kamanda Nyigesa amesema baada ya polisi kuoneshwa eneo ulimofukiwa mwili wa mwanamke huyo waliufukua na kuufanyia uchunguzi na kisha kuukabidhi kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

Watuhumiwa wote watatu watafikishwa mahakamani pindi uchunguzi utakapokamilika.