Idris Sultan afikishwa mahakamani kwa kosa la mtandao

0
1616

Msanii Idris Sultan na wenzake wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na kosa la kuchapisha maudhui mtandaoni bila leseni ya Mamalaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Idris na wenzake wawili, Dokta Ulimwengu na Isihaka Mwinyimvua wamesomewa shitaka lao Wakili wa Serikali, Batrida Mushi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Katika kesi hiyo namba 60 ya mwaka 2020, wakili wa serikali amesema Idris na wenzake wametenda kosa la kurusha maudhui kupitia chaneli ya YouTube pasi na kuwa na leseni ya TCRA kati ya Machi 8, 2016 na Machi 12, 2020 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa hao baada ya kusomewa shtaka lao, wamekana kutenda kosa hilo na Hakimu Shaidi ametoa masharti ya dhamana, kwa kuwataka kuwa na mdhamini mmoja atakaye saini bondi ya shilingi milioni 8, na pia mdhamini huyo awe na barua inayotambulika kisheria pamoja na kitambulisho cha taifa.

Washtakiwa hao wameachiwa kwa dhamana, na kesi hiyo imeahirishwa hadi April 21, 2020 itakapotajwa tena.