Kamati ya Olimpiki Duniani (IOC) imesema michezo ya Olimpiki ya Tokyo iliyopangwa kufanyika mwezi Julai mwaka huu itafanyika kama ilivyopangwa, na haitasogezwa mbele licha ya dunia kuwa katika mapambano dhidi ya homa ya corona.
Licha kutokuahirishwa kwa michezo hiyo, lakini IOC imefuta mbio za Mwenge wa Olimpiki uliokuwa utembezwe kwenye nchi zote wanachama wa kamati hiyo.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania, Filbert Bayi ameliambia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuwa, IOC imezitaka nchi zote kuendelea na maandalizi ya michuano hiyo lakini imepiga marufuku michuano ya mchujo ya kanda.
Mpaka sasa ni asilimia 57 pekee ya wachezaji na timu ndio wamefanikiwa kufikia viwango vya kucheza michuano ya Olimpiki ya Tokyo baadae mwaka huu, huku asilimia 43 wakiwa bado wanasaka nafasi hiyo.