Kamati ya muda kuiongoza Ndanda FC

0
2467

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, -Gelasius Byakanwa ametangaza kuuweka pembeni uongozi wa timu ya mpira wa miguu ya Ndanda FC ya mkoani humo.

Kufuatia hatua hiyo Byakanwa ambaye pia ni mlezi wa timu hiyo ameunda kamati ya muda itakayoisimamia timu hiyo katika mechi 29 zilizobaki katika msimu huu wa Ligi Kuu.

Amesema kuwa pamoja na kuunda kamati hiyo ya muda itakayosimamia timu ya Ndanda FC, mkoa wa Mtwara uko katika mkakati wa kutafuta mfadhili atakayeweza kuisaidia timu hiyo ambayo kwa sasa inashika nafasi ya 16 katika msimamo wa Ligi Kuu.

Kamati hiyo ya watu kumi inaongozwa na Laurent Werema.

Byakanwa amesema kuwa ameamua kufanya hivyo ili kuinusuru timu hiyo ambayo hivi karibuni ilishindwa kusafiri kutoka mkoani Singida kurudi Mtwara kutokana na kukosa fedha za nauli.

Hali hiyo ilisababisha msanii wa kizazi kipya (Bongo Fleva) Hamonize ambaye anatokea mkoani humo na pia ni Balozi wa timu hiyo kuichangia shilingi milioni 3.5 ili iweze kusafiri na kurudi Mtwara.