Serikali yatoa sababu sampuli za Corona kupimwa Dar

0
440

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amesema kuwa sampuli za washukiwa wa virusi vya Corona zinapimwa maabara ya taifa iliyopo jijini Dar es Salaam pekee kwa sababu ndiyo inayokidhi vigezo vya kupima virusi hivyo nchini.

Ummy Mwalimu ametoa kauli hiyo leo kufuatia wananchi wengi kuhoji sababu za serikali kusafirisha sampuli kutoka maeneo mbalimbali kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi badala ya kupimiwi huko huko zinapotokea.

“Kirusi hiki ni ‘highly infectious’ (kina ambukiza kwa kasi), kinapimwa katika maabara maalum ambapo ina ngazi inaitwa ‘biosafety level 3.’ Kwa nchini Tanzania ni Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii tu ambayo ipo ngazi ya tatu katika upimaji wa sampuli za virusi ambavyo vina hatari ya kuambukiza kwa kiasi kikubwa,” amefafanua waziri huyo.

Ameongeza kuwa kabla ya Februari 15 mwaka huu Kusini mwa Jangwa la Sahara maabara mbili tu (Afrika Kusini na Senegal) ndizo zilikuwa na uwezo wa kupima kirusi cha Corona, hivyo kwa Tanzania kuwa na maabara inayoweza kupima kunaonesha kuwa kazi kubwa imefanyika.

Aidha, amewatoa hofu wananchi kuwa wamechukua hatua madhubuti pamoja na kusaini mikataba kuhusu namna ambavyo sampuli zitasafirishwa kuelekea Dar es Salaam, kama ambavyo ilikuwa ikifanyika hata wakati wa Ebola.