Viongozi wa Bara la Afrika wametakiwa kuhakikisha chaguzi mbalimbali zinazofanyika katika mataifa yao zinafanyika kwa kuzingatia kanuni na sheria.
Wito huo umetolewa jijini Dar es salaam na baadhi ya wasomi na wanasiasa wakati wa mdahalo wa wazi wa kumbukizi ya miaka 19 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambapo miongoni mwa mada zilizojadiliwa ni ile inayohusu mienendo ya chaguzi na mustakabali wa mataifa ya Afrika.
Akifungua mdahalo huo, Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Rwekaza Mukandala amesema kuwa nchi nyingi za Bara la Afrika zimekuwa zikifanya chaguzi ambazo hazileti tija katika mataifa yao bali kuchochea migogoro ya kisiasa.
Amesema kuwa jambo kubwa ambalo mataifa ya Afrika yanatakiwa kufahamu ni kuendeleza yale yaliyoasisiwa na waasisi wa mataifa hayo ambao walikuwa na mwelekeo wa kuimarisha demokrasia iliyoleta tija ndani ya mataifa yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, -Joseph Butiku amesema kuwa Watanzania wanatakiwa kufahamu kuwa amani ni jambo la kuzingatiwa katika kipindi cha uchaguzi ili taifa liendelee kuwa na amani na utulivu.