Maporomoko ya udongo yasababisha vifo Uganda

0
2372

Zaidi ya watu thelathini wamethibitika kufa baada ya kutokea kwa maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika eneo la mashariki la Uganda.

Idadi hiyo ya watu waliokufa inatarajiwa kuongezeka kwa kuwa bado watu kadhaa hawajulikani walipo.

Habari kutoka nchini Uganda zinasema kuwa vikosi vya uokoaji vipo katika maeneo yaliyoathiriwa na maporomoko hayo ya udongo na matumaini ni kuwapata watu kadhaa wakiwa hai.

Katika wilaya ya Bududa, watu wengi wamekufa baada ya kufukiwa na vifusi vya udongo pamoja na mawe yaliyosombwa kutoka maeneo ya milimani, ambayo pia yamesababisha kuharibiwa kwa nyumba zote zilizopo kwenye vijiji vitatu vya wilaya hiyo.

Mwaka 2010, takribani watu mia moja walikufa katika tukio kama hilo la maporomoko ya udongo katika wilaya hiyo ya Bududa, huku tukio kama hilo likiripotiwa kutokea kila mwaka katika wilaya hiyo na kusababisha vifo, majeruhi pamoja na uharibifu wa mali.