Mambo 5 ya kuzingatia unapotaka kununua kompyuta

0
2093

Watu wengi hupata changamoto sana wanapotaka kununua tarakilishi (kompyuta) hasa kutokana na ukweli kuwa hawafahamu vitu vya kuzingatia, na hivyo hujikuta wakiishia kuangalia rangi na muonekano wa nje wa kompyuta.

Kuna vitu kadha wa kadha vya kuzingatia wakati unapotaka kununua kompyuta, lakini katika makala hii fupi tutaangazia mambo matano ambayo ukiyazingatia utapata kompyuta ambayo itakufaa kwa matumizi yako.

1.Matumizi yako na bajeti
Hapa tutaangalia vitu viwili ambavyo vyote vinaweza kuathiri kompyuta utakayoinunua. Kwanza tukiangalia matumizi, kutokana na matumizi yako unaweza kuamua kununua kompyuta ya kupakata (laptop) au ya mezani (desktop). Baadhi ya watu ambao kazi zao zinahusisha kuwa maeneo mbalimbali hupendelea laptop zaidi.

Bajeti yako pia itaamua aina ya kompyuta unayotaka kununua. Kila mtu anataka kitu kizuri, bora na chenye uwezo mkubwa, lakini kutokana na uwezo wako wa kifedha, unanunua kile unachokimudu.

2. Processor
Processor ni kifaa ambacho huchakata taarifa zinazopitishwa na mfumo endeshi (OS) wa kompyuta. Hadi sasa processor nzuri zaidi ni Itel Core i7.

3. RAM
Ukubwa wa RAM katika kompyuta unamanisha idadi kubwa ya programu unazoweza kuziendesha kwa wakati mmoja bila kompyuta yako kukwama kwama. Kama utaitumia kompyuta yako kucheza ‘games,’ kuhariri picha au video unahitaji angalau RAM yenye ukubwa wa 16GB, lakini kama ni matumizi yasiyo makubwa 4GB au 8GB inatosha. Pia tambua kwamba unaweza kuongeza ukubwa wa RAM wakati wowote.

4. Hifadhi (Hard Drive)
Unahitaji kompyuta yenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi taarifa zako pamoja na mambo mengine kama vile filamu, tamthilia, muziki, na picha. Unapotaka kununua kompyuta angalau nunua yenye ukubwa wa 500GB ili uweze kuhifadhi vitu vingi zaidi. Hata hivyo kutokana na ongezeko la watu wengi kuhifadhi taarifa zao mitandaoni (cloud storage), unaweza ukanunua kompyuta yenye nafasi ndogo, na taarifa zako ukawa unaziweka sehemu nyingine.

5. Dhamana (Warranty)
Takribani chapa (brands) zote hutoa waranti ya kipindi fulani kwa mteja anayenunua kompyuta, hivyo kikubwa hapa ni kuangalia chapa ambayo ina waranti bora zaidi, ili kujihakikishia usalama wa kifaa chako.