Lema mikononi mwa mkurugenzi wa mashtaka

0
356

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga amesema kuwa ofisi yake itamchukulia hatua Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Godbless Lema,  kwa kutoa taarifa za uongo  kuhusu mauaji ya watu 14 wilayani Manyoni mkoani Singida, hali inayochochea chuki na kuhatarisha amani ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Mganga amemtaka Lema ajitokeza na kumueleza kuhusu mauaji ya watu hao,  na ni lini alitoa taarifa za mauaji hayo ambapo polisi walishindwa kuzifanyia kazi kama alivyodai.

DPP amewataka Watanzania kuelewa na kuwa watulivu pindi ofisi yake itakapochukua hatua dhidi ya mbunge huyo, na kwamba ofisi hiyo itamchukulia hatua mtu yeyote bila kujali chama chake, rangi, kabila ama cheo chake ambaye atafanya jambo lolote linalohatarisha amani ya nchi.

Ametoa wito kwa Wanasiasa nchini kutotumia kivuli cha siasa katika kuvuruga amani na badala yake wafanye siasa zenye staha.

Lema anadaiwa kusambaza taarifa za mauaji ya watu 14 wilayani Manyoni, wakati alipokua akizungumza katika mazishi ya aliyekuwa katibu wa CHADEMA jimbo la Singida Mashariki Alex Joas, ambaye mwili wake ulikutwa kando ya barabara ukiwa na majeraha kichwani.