Mashinji atoka Segerea

0
226

Aliyekua Katibu Mkuu wa Chama cha  Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye baadae alihamia Chama Cha Mapinduzi( CCM) Dkt Vicent Mashinji, ameishukuru CCM kwa kumlipia faini ya shilingi milioni 30 aliyotakiwa kulipa baada ya kupatikana na hatia katika makosa 12.

Akizungumza mara baada ya kuruhusiwa kutoka katika gereza la Segerea jijini Dar es salaam kufuatia kukamilika kwa taratibu za faini, Dkt Mashinji amesema ahadi yake kwa CCM ni kuendelea kuitumikia kwa uaminifu chama hicho.
 
Mapema hii leo, Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC)- Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, Humphrey Polepole alifika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kumlipia faini ya shilingi milioni 30 Dkt Mashinji.

Hapo jana Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba aliwahukumu viongozi waandamizi wa CHADEMA pamoja na Dkt Mashinji kulipa faini ya jumla ya shilingi milioni 350 au kifungo cha miezi mitano jela kwa kila kosa, baada ya kuwakuta na hatia katika makosa hayo kumi na mawili.

Katika mgawanyo wa faini hiyo, Dkt Mashinji alitakiwa kulipa shilingi milioni 30.