Corona yaahirisha mchezo wa Man City na Arsenal

0
1126

Mchezo wa Ligi Kuu ya England kati ya Manchester City dhidi ya Arsenal uliokuwa umepangwa kufanyika leo umeahirishwa kutokana na hofu ya virusi vya Corona, baada ya mmiliki wa klabu ya Olympiakos, Evangelos Marinakis kuambukizwa virusi hivyo.

Klabu ya Arsenal imeeleza kuwa Marinakis (52) alikutana na baadhi ya wachezaji wakati klabu hiyo ya England ilipocheza na Olympiakos katika mchezo wa Ligi ya Europa wiki mbili zilizopita.

Wakati mchezo huo wa ligi ukiahirishwa, UEFA imetupilia mbali ombi la klabu ya Wolves la kuahirisha mchezo wake wa mzunguko wa 16 bora wa Ligi ya Europa dhidi ya Olympiakos unaotarajiwa kuchezwa Machi 12 mwaka huu.

Shirikisho la Soka nchini England limesema halitoahirisha mchezo mwingine wowote kwani hatua madhubuti tayari zimechukuliwa kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo vinavyoitikisa dunia.

Hadi sasa tayari kumethibitishwa kuwapo visa 382 vya virusi vya corona nchini Uingereza, na watu sita wamefariki dunia.

Virusi hivyo vimeathiri michezo maeneo mbalimbali duniani ambapo nchini Italia ligi kuu, Serie A, imeahirishwa, wakati nchini Ufaransa na Hispania baadhi ya michezo ikifanyika bila mashabiki kuwemo uwanjani.