Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa barabara ya muda kwenye eneo la daraja la Kiyegea linalounganisha mikoa ya Morogoro na Dodoma na kusema kazi inaenda vizuri sababu hakuna tena msongamano wa magari kama ilivyokuwa wiki iliyopita.
Waziri Mkuu ametoa agizo wakati akizungumza na watendaji wa wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na viongozi wa mkoa wa Morogoro, mara baada ya kutembelea eneo hilo na kukagua ujenzi wa barabara ya muda ili kurejesha mawasiliano na mikoa mingine.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wa mikoa yote nchini wanapaswa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa madaraja yote ili kujiridhisha na usalama wake.
“Nimekuja kuona kazi inaendeleaje, nimekuta msongamano wa magari hakuna kama ilivyokuwa wiki iliyopita, ile diversion (barabara ya mchepuko) imesaidia kuondoa msongano uliokuwepo,” amesema Waziri Mkuu.
Katika ukaguzi huo Waziri Mkuu amebaini kuwa Meneja wa TANROADS, mkoa wa Morogoro, Mhandisi Godwin Andalwisye ambaye aliagiza arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine, bado alikuwepo kwenye eneo la tukio akiendelea na kazi.
“Uamuzi niliochukua wa kumuhamisha Meneja wa TANROADS mkoa wa Morogoro ulikuwa sahihi kwa sababu huyu Bwana anaonekana hawezi kazi ya kusimamia wengine, fedha ya ukaguzi ipo, ya ujenzi ipo, halafu kazi haifanyiki, Kazi ya kusupervise haiwezi, kwa hiyo ateuliwe Meneja mwingine,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Akijibu hoja hiyo Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandishi Patrick Mfugale amesema amemuacha Mhandisi Andalwisye aendelee kuwepo kwenye eneo la ujenzi kwa sababu ya utalaamu wake kwenye madaraja.
“Ulishatoa maelekezo kuwa aondolewe, na wa kumhamisha ni mimi, tunatumia tu utaalmu wake”, amesema Mhandisi Mfugale.
Alipoulizwa kama ameshateua Meneja mwingine wa TANROADS kwa mkoa wa Morogoro, Mhandisi Mfugale alikiri kwamba bado hajamteua mtu mwingine.
Machi Nne mwaka huu Waziri Mkuu Majaliwa alikatisha ziara yake mkoani Tanga na kutembelea eneo hilo ambako alishuhudia mlundikano wa magari na abiria, hali ambayo haikumfurahisha na kuagiza Meneja wa TANROADS mkoa wa Morogoro arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine mara moja kwa sababu ya kuzembea kutimiza wajibu wake.