Maofisa watatu wasimamishwa kazi Korogwe

0
142

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mweka Hazina wa halmashauri ya Mji Korogwe, -Subilaga Kapange pamoja na maafisa wengine wawili wanaosimamia ukusanyaji wa mapato katika kituo cha mabasi cha Korogwe baada ya kushindwa kuwasilisha mapato serikalini.

Waziri Mkuu ametangaza uamuzi huo wakati wa mkutano wake na watumishi wa halmashauri ya Mji Korogwe na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa TTC, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Tanga.

Amesema halmashauri ya Mji Korogwe imejenga kituo cha mabasi lakini makusanyo yake hayafikishwi serikalini, huku baadhi ya wazabuni waliopewa kazi hiyo wakiwa hawana hata mikataba, jambo linalochangia halmashauri hiyo kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji. 

“Mnakusanya fedha na kuziweka mfukoni, hazipelekwi benki mnazitumia kwa matumizi yenu binafsi na kuna siku inaonyesha hamjakusanya chochote, hatuwezi kuvumia hali hii hawa wote wakamatwe na wawekwe ndani na hii iwe funzo kwa waweka hazina wote nchini”, amesisitiza Waziri Mkuu.

Maofisa wengine waliosimamishwa kazi na Waziri Mkuu Majaliwa ni Meneja wa kituo cha mabasi Majid Salehe na msaidizi wake.

“Kuna siku kituo kinakusanya sh 51, 000 tu licha ya mabasi mengi kupita, hata hivyo februari 27, 2020 hawakukusanya kiasi chochote inamaana hakuna basi lililopita, februari 28, 2020 walikusanya sh 785,000 na februari 29, 2020 walikusanya mara mbili sh 500,000 na sh 990,000 lakini fedha zote hizo hazikupelekwa benki
baada ya kusikia nakuja Korogwe machi 4, 2020 walikusanya sh. milioni 11 na kuzipeleka benki na risiti ninazo, siku zote hakuna risiti kwa sababu fedha hazipelekwi benki na wakusanyaji wengine ni marafiki zao hivyo hata wasipokusanya hakuna wa kuwauliza,” amefafanua Waziri Mkuu.

Amesema serikali haiwezi kulea watumishi wa aina hiyo, hivyo amemuelekeza Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Korogwe, – Nicodemus Bei ahakikishe anakuwa makini katika kufuatilia zinakopelekwa fedha za mapato yanazokusanywa kwenye eneo lake.