Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli amekabidhi viti mwendo mia mbili na kumi kwa baadhi wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuwagawia watoto wenye uhitaji kwenye majimbo yao.
Viti hivyo vimekabidhiwa kwa Naibu Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam.
Akipokea viti hivyo kwa niaba ya wabunge hao, Naibu Spika amemshukuru Mama Janeth Magufuli kwa kuendelea kuwasaidia wananchi wenye uhitaji wakiwemo watoto wenye ulemavu na wazee na kwamba kitendo hicho ni cha kizalendo na chenye kutia moyo.
Dkt Tulia ameongeza kuwa, katika kuwasaidia wazee na watoto wenye ulemavu, Mama Magufuli amekuwa mfano wa kuigwa kwa wanawake nchini kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii ya watu wenye uhitaji.
Mama Magufuli ambaye ametoa msaada huo wa viti mwendo kwa watoto wenye ulemavu zikiwa zimesalia siku chache kabla ya maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani machi nane mwaka huu, amewashukuru wabunge wote walioitikia wito wake wa kupokea msaada huo kwa ajili ya kuwagawia watoto wenye uhitaji katika majimbo yao.
“Kama mjuavyo kila tarehe nane mwezi Machi ni Siku ya Wanawake
Duniani, hivyo basi nikiwa miongoni mwa wanawake nimeguswa na
kuamua kusherehekea siku hii muhimu kwetu kwa kutoa zawadi ndogo ya viti mwendo kwa waheshimiwa wabunge ili wawafikishie
wanangu wenye uhitaji kwenye majimbo yao kwa urahisi zaidi, kwani wao ndio wawakilishi wa wananchi”, amesema Mama Magufuli.