Shirika la ndege la Ethiopia kutositisha safari kwenda China

0
584

Kwa mara nyingine tena shirika la ndege la Ethiopia limekataa kusitisha safari zake za ndege kwenda nchini China, licha ya kuwepo kwa shinkizo la kulitaka kufanya hivyo kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Mkurugenzi wa shirika hilo Tewolde Gebremariam amesema kuwa, kusitisha safari za ndege kwenda China si suluhisho la kukabiliana na maambukizi ya corona na kwamba si sahihi kuitenga nchi hiyo kutokana na mlipuko wa Virusi hivyo.

Tewolde amesema kuwa, shirika hilo la ndege la Ethiopia kama yalivyo mashirika mengine ya ndege limeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na mlipuko wa virusi vya corona nchini China.

Mpaka sasa mashirika kadhaa ya ndege barani Afrika yamesitisha safari zake za ndege kwenda nchini China ikiwa ni  pamoja na shirika la ndege la Afrika Kusini, shirika la ndege la Mauritius, shirika la ndege la Misri na shirika la ndege la Kenya.

Kwa mujibu wa muungano wa mashirika ya ndege ya Kimataifa, mashirika ya ndege ya Afrika yamepata hasara ya dola milioni mia nne za Kimarekani tangu kutokea kwa mlipuko wa virusi vya corona nchini China.