Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko ameufunga mgodi wa kokoto wa Tan- Turk ulipo katika kijiji cha Mindutulieni wilayani Bagamoyo mkoani Pwani hadi hapo mmiliki wa mgodi huo atakapowalipa fidia wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Naibu Waziri Biteko ametangaza kuufunga mgodi huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakazi wa kijiji hicho ambao wamedai kuwa shughuli za ulipuaji wa baruti katika miamba zinazofanywa katika mgodi zimekua zikisababisha mawe makubwa kuruka na kuangukia katika makazi ya watu, jambo linalohatarisha maisha yao.
Akizungumza mara baada ya kukagua mgodi huo wa kokoto wa Tan- Turk , Naibu Waziri Biteko amemuagiza mmiliki wake kutofanya shughuli zozote hadi hapo atakapozilipa fidia kaya zaidi ya Thelathini zilizopo katika eneo la mgodi.
Akiwa katika mgodi huo, Naibu Waziri Biteko pia ameelezea kutoridhishwa na utunzaji wa kumbukumbu za kiwango cha kokoto kinachouzwa ndani ya mgodi huo, hali inayosababisha serikali kukosa mapato.