Rais Magufuli akutana na Maalim Seif, Lipumba na Mbatia

0
232

Rais John Magufuli kwa nyakati tofauti amekutana na kufanya mazungumzo na Wanasiasa watatu ambao ni Maalim Seif Sharif Hamad, Profesa Ibrahimu Lipumba na James Mbatia Ikulu jijini Dar es salaam.

Maalim Seif Sharif na Rais John Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam

Baada ya mazungumzo hayo Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mstaafu amesema  kuwa , yeye na Rais Magufuli wamezungumzia masuala ya kudumisha amani, usalama na upendo kwa watu wote na ameelezea kufurahishwa na dhamira ya Rais  kukutana na viongozi mbalimbali na kujadiliana mambo yenye maslahi kwa Taifa.

Kwa upande wake Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) amempongeza Rais Magufuli kwa ahadi yake kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa huru na wa haki na amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na serikali  katika kupambana na rushwa, kudhibiti matumizi ya serikali, kulinda na kutumia vizuri rasilimali za Taifa, kuboresha elimu na kuimarisha uchumi.

Ametoa wito kwa Watanzania wote kuweka uzalendo mbele, kudumisha amani na utawala bora na amewataka wanachama wote wa CUF kujiandaa kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo.

Prof Ibrahim Lipumba akizungumza Ikulu Jijini Dar es salaam na Rais Dkt. John Magufuli


Profesa Lipumba amewakosoa wanasiasa wanaopinga kila jambo linalofanywa na serikali na kufafanua kuwa serikali ya awamu ya Tano imetekeleza vizuri mambo mengi yaliyokuwa yakisemwa na vyama vya upinzani, hivyo sio sawa kwa vyama hivyo kupinga jambo vililotaka litekelezwe na linatekelezwa.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha NCCR Mageuzi  James Mbatia pamoja na kufurahishwa na dhamira ya Rais Magufuli juu ya uchaguzi mkuu kuwa huru na wa haki, ametaka wanasiasa nchini kuacha kuchochea mambo hasi dhidi ya Taifa na badala yake waungane kuendeleza mambo mazuri yanayofanywa na serikali.


Mbatia ametoa wito kwa wanasiasa na Watanzania wote kuweka mbele maslahi ya Taifa badala ya kukumbatia mambo yenye maslahi binafsi.

James Mbatia na Rais Dkt John Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam