Rais John Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa Msikiti mkubwa wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) unaojengwa Kinondoni jijini Dar es salaam.
Msikiti huo unajengwa kwa ufadhili wa Mfalme Mohammed VI wa Morocco, baada ya kuombwa na Rais Magufuli alipofanya ziara rasmi nchini mwezi oktoba mwaka 2016.
Akiongozwa na Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir, Rais Magufuli amejionea kazi za ukamilishaji wa jengo jipya la msikiti na jengo la ofisi ya Taasisi ya Mfalme Mohammed VI wa Morocco zikiendelea kukamilishwa, na ameelezea kufurahishwa na ubora na uzuri wa Msikiti huo.
Rais Magufuli amemshukuru Mfalme Mohammed VI wa Morocco kwa kutekeleza ombi la kuwajengea Waumini wa dini ya Kiislamu Msikiti mkubwa kuliko yote hapa nchini, na amempongeza Mufti wa Tanzania na Waislamu wote kwa kujengewa nyumba nzuri ya Ibada.
Mufti wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwajali Waislamu na kuwaombea msaada wa kujengewa Msikiti huo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 97.
Akiwa na viongozi wenzake wa BAKWATA, Mufti ameongoza Dua ya kumuombea Rais Magufuli na kuliombea Taifa ili Mwenyezi Mungu aliepushe dhidi ya virusi vya corona, kudumisha amani na utulivu na kuombea uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu ufanyike kwa amani na utulivu.