Baraza la Wadhamini wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) limewaagiza watendaji na viongozi wote wa chama hicho na Jumuiya zake wa ngazi mbalimbali kuhakikisha katika maeneo yao hakuna mali yoyote ya chama au Jumuiya inayouzwa, kukodishwa, kumilikishwa au kuhaulishwa kwa mtu yeyote au chombo kingine bila idhini ya baraza hilo.
Agizo hilo limetolewa na Baraza hilo chini ya Mwenyekiti wake Anna Abdalla lilipokutana katika ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM Lumumba jijini Dar es salaam, ikiwa ni mara ya kwanza tangu liteuliwe Julai Kumi mwaka huu.
Pamoja na mambo mengine, Baraza hilo la Wadhamini wa CCM limeipitia kwa kina na kuanza kuifanyia kazi ripoti ya Tume ya kuhakiki mali za chama na Jumuiya zake kwa lengo la kuchambua na kuzifanyia kazi changamoto na mapendekezo yote ya tume yanayohusu mali za CCM.
Kwa mujibu wa katiba ya CCM ya mwaka 1977, Baraza la Wadhamini wa CCM ndilo lenye jukumu la kumiliki na kusimamia mali zote zinazoondosheka na zisizoondosheka za Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake.
Baraza hilo limeelezea kubaini uwepo wa mikataba isiyo na tija, uuzaji, uporaji na uvamizi wa mali za CCM kinyume na katiba ya chama hicho na hivyo kuwaonya watendaji na viongozi wote kuacha mara moja vitendo hivyo.
Kufuatia hali hiyo, Baraza la Wadhamini wa CCM limeziagiza mamlaka zote husika za chama hicho na Jumuiya zake kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watendaji na viongozi wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uuzaji wa mali za chama hicho ama Jumuiya zake bila kibali.