Collin Sixton ameiongoza vyema Cleveland Cavaliers kwa kuifungia alama 28 katika dakika 36 alizocheza na kuwasaidia mabingwa hao wa zamani kupata ushindi wa alama 108 kwa 94 dhidi ya Philadelphia 76ers kwenye ligi ya kulipwa ya mpira wa kikapu nchini Marekani (NBA).
Licha ya Shake Milton kuifungia Sixers alama 20 na kucheza rebounds nne (mipira iliyorudi) huku Forkan Korkmaz akifunga alama nyingine 14, bado hazikutosha kuwapa ushindi na sasa wanapoteza mchezo wa 23 kwa msimu huu.
Katika matokeo ya baadhi ya michezo mingine, Washington Wizards wamepata ushindi wa alama 110 kwa 106 dhidi ya Brooklyn Nets katika mchezo ambao Bradley Beal amefunga alama 30, wakati New York Knicks wakinyukwa alama 107 kwa 101 na Charlote Hornets, huku Atlanta Hawks wakila mweleka wa alama 130 kwa 120 mbele ya Orlando Magic na Minnesota Timberwolves wakiitandika Miami Heat alama 129 kwa 126.