Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema kuwa hatua iliyochukuliwa na Bunge la Tanzania katika kufanya mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa, sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali, na ile ya vyombo vya habari ina lengo la kuimarisha uwajibikaji na uwazi.
Profesa Palamagamba Kabudi ameyasema hayo huko Geneva, Uswisi alipokua akihutubia kikao cha 43 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kuihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa Tanzania inaheshimu na itaendelea kuheshimu haki zote binadamu.
Amewaambia washiriki wa kikao hicho kuwa, mwaka huu Tanzania itafanya uchaguzi wake mkuu wa sita tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, na kuwahakikishia kuwa uchaguzi huo utakuwa wa uwazi, huru, na wa haki.
Kuhusu sheria mpya ya huduma za vyombo vya habari na haki ya kupata taarifa, Waziri Kabudi amesema kuwa lengo la sheria hiyo ni kuimarisha, kulinda, na kuweka mazingira bora zaidi kwa waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa usalama na kwa kuzingatia taaluma pamoja na kuwawezesha kupata haki zao.