Waliotoa rushwa TRA wafikishwa mahakamani

0
362

Raia wawili wa China akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya International Ronglan iliyoko Mafinga mkoani Iringa, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam wakikabiliwa na kosa la kutoa rushwa na kukwepa kodi ya zaidi ya Shilingi Bilioni Moja.
 
Raia hao ni Zeng Ronglan na Ou Ya,  wote wakazi wa Mafinga mkoani Iringa.
 
Akisoma hati ya mashitaka ya watuhumiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Huruma Shaidi, wakili wa Serikali Ipyana Mwakatobe amesema kuwa, washitakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo Februari 24 mwaka huu katika eneo la Makao Makauu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
 
Katika shitaka la kujihusisha na utoaji wa rushwa, Wakili Mwakatobe amesema kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa kutoa Dola Elfu Tano za Kimarekani kwa Kamishna Mkuu wa TRA Dkt Edwin Mhede wakati wakijua ni kosa.
 
Katika shitaka la ukwepaji wa kodi, ZENG na mwenzake wanadaiwa kumshawishi Kamishna Mkuu wa TRA ili kuisamehe Kampuni ya International Ronglan kutokulipa kodi ya zaidi Shilingi Bilioni Moja.
 
Washitakiwa hao wamekiri makosa yao na kurejeshwa rumande hadi tarehe 26  mwezi huu kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali juu ya kesi inayowakabili.