Mahakama Kuu nchini Lesotho inatarajiwa kutoa uamuzi kama Waziri Mkuu wa nchi hiyo Thomas Thabane anaweza kushtakiwa akiwa madarakani kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha mke wake wa kwanza Lipolelo Thabane ama la.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mwanasheria wa Thabane kupinga kitendo cha mteja wake kutaka kushtakiwa akiwa madarakani.
Awali Mwanasheria huyo alitaka shauri hilo kupelekwa Mahakama ya Katiba na sio Mahakama kuu, lakini mahakimu walilipeleka katika Mahakama Kuu ya Lesotho.
Hivi karibuni Waziri Mkuu huyo wa Lesotho amesikika akisema kuwa, ataachia wadhifa huo mwezi Julai mwaka huu kufuatia shinikizo kutoka kwenye chake ambako ametakiwa kuondoka madarakani haraka iwezekanavyo kufuatia tuhuma zinazomkabili.
Thabane mwenye umri wa miaka Themanini, anatuhumiwa kuhusika na mauaji ya Lipolelo, siku mbili kabla ya kuapishwa kushika wadhifa huo wa Uwaziri Mkuu mwaka 2017.
Mke wa sasa wa Thabane, – Maesaiah Thabane naye anashitakiwa kwa kuhusika na mauaji hayo ya mke mwenzake Lipolelo, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi nje kidogo ya mji mkuu wa nchi hiyo Maseru.