Profesa PLO ataka nchi za Afrika zijifunze kutoka Tanzania

0
327

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na msomi na Mwanamajumui wa Afrika Profesa Patrick Lumumba maarufu kama PLO, Ikulu jijini Dar es salaam.

Rais Magufuli na Profesa PLO Lumumba ambaye ni raia wa Kenya wamezungumzia masuala mbalimbali yahusuyo juhudi za Afrika katika kuimarisha uchumi kwa kutumia rasilimali zake na pia wajibu wa Waafrika na viongozi wao katika kuimarisha huduma za kijamii na kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Amempongeza Profesa PLO Lumumba kwa juhudi zake za kueleza waziwazi makosa yanayosababisha nchi za Afrika kubaki nyuma kiuchumi, kijamii na kisiasa, wajibu wa viongozi na wananchi wa Afrika katika kukabiliana na changamoto zinazozikabili nchi zao na mapenzi yake makubwa kwa Afrika.

“Mimi sijawahi kukutana nawe kabla, lakini nakusikia na kukuona kupitia vyombo vya habari jinsi unavyopaza sauti kuhusu Bara la Afrika, nakupongeza kwa juhudi hizo, na ninafarijika kwamba unaisemea vizuri Afrika” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia amemueleza Mwanamajumui huyo wa Afrika juhudi ambazo Serikali inazifanya katika kujenga uchumi imara wa kujitegemea ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa Bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme, ujenzi wa barabara na madaraja makubwa na  madogo pamoja na kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari.

Kwa upande wake Profesa  PLO Lumumba amemshukuru Rais Magufuli kwa kutenga muda wake kuzungumza nae, na amempongeza kwa juhudi kubwa alizozionyesha katika kipindi kifupi cha uongozi wake wa miaka minne ambapo ameonyesha mfano wa namna ya kupigania rasilimali za nchi ikiwemo madini, kujenga nidhamu ya utumishi Serikalini, kuimarisha uchumi, kupambana na wizi wa mali za umma, rushwa na ufisadi.

Amesema inafaa kwa nchi za Afrika kujifunza mambo yanayofanyika Tanzania kwa sasa na amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Waafrika kujiamini na kuchukua hatua madhubuti za kuwaondoa katika hali ya sasa ambapo rasilimali zake zinachukuliwa na mataifa ya nje ilihali wananchi wake wakikabiliwa na changamoto mbalimbali.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na Mwakilishi wa Kansela wa Ujerumani anayeshughulikia masuala ya Afrika Guenter Nooke, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Nooke amewasilisha kwa Rais Magufuli ujumbe wa Kansela wa Ujerumani, –  Angela Merkel na pia ameelezea kufurahishwa kwake na hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa hapa nchini ikilinganishwa na alipokuja miaka iliyopita.

Pia amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali katika kupambana na rushwa na kuimarisha uchumi ambapo ameahidi kuwa Ujerumani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji na biashara na masuala mengine ya kijamii.

Kwa upande wake Rais Magufuli amemuhakikishia Kansela wa Ujerumani kuwa Tanzania ipo tayari kuuendeleza na kuukuza zaidi uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na Ujerumani na inawakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kuwekeza nchini.