Korea Kaskazini yahofia corona

0
406

Korea Kaskazini imewaweka kwenye karantini raia 380 wa kigeni walioingia nchini humo, ikiwa ni moja ya njia za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Wengi wa raia hao wa kigeni ni Wanadiplomasia ambao wamewekwa kwenye karantini katika Mji Mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang.

Awali, raia wengine wa kigeni zaidi ya 200 waliwekwa kwenye karantini kwa muda wa siku 30 na baadae kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao baada ya kubainika kuwa hawana virusi hivyo vya corona.

Maafisa wa afya Korea Kaskazini wamesema kuwa, hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyegundulika kuwa na virusi hivyo vya corona nchini humo na kwamba raia wote wa kigeni wanaoingia nchini humo wataendelea kuwekwa kwenye karantini ili kuhakikisha virusi hivyo haviingia nchini humo.

Kwa upande mwingine, huko Korea Kusini tayari watu saba wamethibitika kufariki dunia kutokana na virusi hivyo, na wengine 763 wameugua homa hiyo.

Virusi hivyo vilivyoanzia katika Mji wa Wuhan nchini China, pia vimeathiri nchi nyingine 29 duniani.