Mahakama yasisitiza Lissu afikishwe mahakamani

0
215

Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili aliyekua Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Tundu Lissu umeomba muda wa wiki mbili kupitia maombi yaliyowasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo jijini Dar es salaam na wadhamini wa mshitakiwa huyo.
 
Hii leo ilitarajiwa Mahakama hiyo kupitia vifungu vya sheria ili kuona kama sheria zinaruhusu wadhamini hao kuomba kibali cha kukamatwa kwa mshtakiwa huyo na wao kujitoa kwenye udhamini.
 
Wakili wa Serikali, – Wankyo Simon amedai mahakamani hapo kuwa, upande wa mashitaka unahitaji muda wa kutosha kuyapitia maombi ya wadhamini hao ikiwemo kiapo kinzani juu ya shauri hilo.
 
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Thomas Simba amesisitiza wadhamini hao kumfikisha Lissu mahakamsni hapo, kwani maombi yao hayawezi kusimamisha kesi isiendelee wala kutengua amri ya  kesi ya msingi inayomkabili mshitakiwa huyo.
 
Wadhamini wa mshitakiwa Lissu ni Ibrahim Ahmed na Robert  Katula wote wakazi wa jiji la Dar es salaam.
 
Hakimu Mkazi Mkuu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi machi Kumi  mwaka huu itakapotajwa tena.