NEC yaongeza muda wa uboreshaji daftari la wapiga kura Dar es Salaam

0
332

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kuongeza muda wa siku tatu katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa mkoa wa  Dar es salaam, ambalo lilikua lifikie ukomo wake hii leo.

Mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Dkt Wilson Mahera amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa, kwa sasa zoezi hilo litafikia ukomo tarehe 23 mwezi huu na baada ya hapo muda hautaongezwa tena.

Amesema kuwa NEC imeamua kuongeza muda huo baada ya kubaini kuwa katika awamu ya kwanza ya zoezi la uboreshaji iliyoanza tarehe 14 mwezi huu kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, kwa mkoa wa Dar es Salaam wananchi hawakujitokeza kuboresha taarifa zao kama ilivyotarajiwa.

NEC imeongeza kuwa katika siku zote za nyongeza, vituo vya kujiandikisha vitaendelea kufunguliwa saa mbili asubuhi hadi saa 12 jioni.

Dkt Mahera amewataka wakazi wa mkoa wa Dar es salaam kutumia muda huo wa nyongeza kuhakikisha taarifa zao zinaboreshwa katika saftari la kudumu la wapiga kura.