MAT yataka taaluma ya Udaktari iheshimiwe

0
168

Rais wa Chama Cha Madaktari Tanzania (MAT) Dkt Elisha Osati amemuomba Raia John Magufuli kutoa maelekezo kwa viongozi mbalimbali ya namna ya kufuata taratibu pindi inapotokea daktari amefanya kosa lolote linalohusu taaluma yake.

Dkt Osati ametoa ombi hilo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wa chama hicho na Rais Magufuli, mkutano unaofanyika pamoja na maadhimisho ya siku ya Madaktari Kitaifa kwa mwaka huu.

Amesema kuwa, kwa muda mrefu madaktari wamekua hawafurahii kitendo cha baadhi ya wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na viongozi wengine wa kisiasa cha kuamuru wao kuwekwa ndani pindi yanapotokea makosa mbalimbali yanayowahusu.

Dkt Osati amesisitiza kuwa kitendo hicho kimekua ni changamoto kubwa katika utendaji wao wa kazi wa kila siku kwa kuwa kinaondoa heshima ya taaluma ya Udaktari.

Ameshauri pindi linapotokea kosa la kitaaluma ufuatwe utaratibu ambao upo na unaoeleweka, ili haki itendeke kwa pande zote mbili ambazo ni mlalamikaji na mlalamikiwa.

Kauli mbiu ya mkutano huo wa Chama Cha Madaktari Tanzania kwa mwaka huu pamona na maadhimisho hayo ya Siku ya Madaktari Kitaifa ni hatua zetu kuelekea huduma bora za afya kwa wote nchini Tanzania.

Mkutano huo wa MAT unafanyika wakati chama hicho kikiwa kimetimiza miaka 55 tangu kuanzishwa kwake.