Waziri Mkuu wa Lesotho atakiwa kujiuzulu leo

0
364

Chama tawala nchini Lesotho kimemtaka waziri mkuu kujiuzulu leo Februari 20, 2020, ikiwa ni siku 2 tu tangu mkewe wa sasa aliposhtakiwa kwa mauaji ya mkewe wa awali.

Mke wa sasa wa Waziri Mkuu Thomas Thabane, Maesaiah Thabane (42) alifikishwa mahakamani Februari 18 mwaka huu na kushtakiwa kuhusika katika mauaji ya mke aliyemtangulia, ambaye aliuawa siku 2 kabla ya mumewe hajaapishwa mwaka 2017.

Chama cha All Basotho Convention (ABC) kilikutana hivi karibuni na kukubaliana kuwa siku ya mwisho kwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 80 kujiuzulu ni leo Alhamisi.

“Hatuwezi kuendelea kuwa nae madarakani, na tunafanya hili tukiamini ni kwa manufaa ya wengi,” msemaji wa chama hicho, Montoeli Masoeta amesema.

Awali chama hicho kilimsihi kiongozi huyo kujiuzulu baada ya uchunguzi wa polisi kubaini kuwa namba yake ya simu ya mkononi ilitumika kuwasiliana na mtu aliyekuwa eneo la mauaji. Licha ya kuahidi kuwa angefanya hivyo, lakini hajatekeleza.

Lipolelo Thabane (58) aliuawa na watu wasiofahamika Juni 2017, na tayari waziri mkuu amehojiwa kuhusu tukio hilo.