Hukumu ya kesi ya Mtendaji Mkuu wa Jamii Forum yashindwa kutolewa

0
125

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo jijini Dar es salaam, leo imeshindwa kutoa hukumu juu ya kesi inayomkabili mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa mtandao wa Jamii Forum, Maxence Melo baada ya hakimu anayeendesha shauri hilo kutohudhuria mahakamani hapo.

Kesi hiyo ilitarajiwa kutolewa hukumu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu  wa mahakama hiyo Thomas Simba.

Awali Wakili wa Serikali Faraji Nguka mbele ya hakimu mkazi Mkuu Huruma Shaidi aliomba kuahirishwa kwa kesi hiyo kwa madai  kuwa Hakimu anayeiendesha amepata udhuru, hivyo mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kutolewa hukumu.
 
Maxence Melo anakabiliwa na mashitaka matatu ikiwemo kushindwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi Nchini na kuharibu uchunguzi kinyume na sheria.

Kwa mara kwanza Melo alifikishwa katika Mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka yake Disemba 16 mwaka 2016.

Hata hivyo Hakimu Mkazi Mkuu wa Kisutu Shaidi Huruma ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili Mbili mwaka huu itakapopelekwa tena mahakamani hapo kwa ajili ya kutolewa uamuzi.

Melo yupo nje kwa dhamana, na kwa mujibu wa sheria kutokana na kesi inayomkabili haruhusiwi kutoka nje ya nchi bila ruhusa maalumu ya mahakama.