Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo jijini Dar es salaam, imemkuta na kesi ya kujibu Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama Cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe katika kesi ya uchochezi ya mwaka 2018 inayomkabili.
Uamuzi huo umetolewa hii leo na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi baada ya kupitia majumuisho ya pande zote mbili yaliyowasilishwa mahakamani hapo wiki mbili zilizopita.
Katika kesi ya msingi, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu yote ya uchochezi, anayodaiwa kuyatenda Oktoba 28 mwaka 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho yaliyopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Katika shtaka la kwanza, inadaiwa siku hiyo akiwa katika mkutano huo kwa nia ya kuleta chuki miongoni jamii dhidi ya jeshi la polisi nchini, alitoa maneno ya uchochezi.