Kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili mwandishi wa habari Erick Kabendera imeshindwa kuendelea hii leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo jijini Dar es salaam, baada ya Hakimu anayesikiliza kesi hiyo kupata dharura.
Kesi hiyo imeshindwa kuendelea huku Kabendera tayari akiwa amewasilisha ombi kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) la kukiri na kuomba msamaha juu tuhuma zinazomkabili.
Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon amemueleza Hakimu Mkazi Vicky Mwaikambo kuwa, shauri hilo liliitishwa kwa ajili ya kutajwa.
Baada ya kueleza hayo Wakili Wankyo ameomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine, ambapo wakili wa upande wa utetezi Reginald Martin ameiomba Mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Kisutu kupanga tarehe ya karibu kwa ajili ya kutaja kesi hiyo.
Hata hivyo Hakimu Mwaikambo ameahirisha kesi hiyo hadi tarehe 24 mwezi huu.
Katika hatua nyingine Mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi ya Uhujumu Uchumi na utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Dickson Maimu na Wenzake.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi wa sheria Sabina Raymond, Xavery Kayombo aliyekuwa Meneja Biashara wa NIDA, Evelyne Momburi na ofisa usafirishaji George Ntalima.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi Nne na Tano mwaka huu.