Gabon yafungia mipaka abiria wa China

0
367

Serikali ya Gabon imetangaza kutoruhusu abiria wanaotoka China kuingia nchini humo, ikiwa ni jitihada za kuzuia kuenea kwa virusi vya homa ya Corona.

Taarifa iliyotolewa na Serikali ya Gabon hivi karibuni imeeleza kuwa, hadi sasa hakuna kisa chochote cha virusi hivyo kilichoripotiwa nchini humo.

“Kutokana na kasi ya kusambaa kwa virusi hivi mbali na vilipoanzia, serikali imeamua kuimarisha ulinzi na kuzuia abiria kutoka China hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo,” imeeleza taarifa hiyo ya serikali.

Hatua ya kutoruhusu abiria wanaotoka China kuingia Gabon inaelezwa kuwa itaathiri uchumi wa nchi hiyo kwa kuwa maelfu ya raia wa China wanafanya kazi nchini humo katika sekta za mafuta, madini na mbao, sekta ambazo zimekua zikichangia kwa kiwango kikubwa kwenye uchumi wa Taifa hilo.

Raia 93 wa Gabon wanaishi katika mji wa Wuhan nchini China, mji ambao mlipuko wa virusi vya Corona ulipoanzia, lakini hakuna yeyote kati ya hao aliyeripotiwa kuambukizwa.