Nyamapori sasa kuuzwa kihalali mabuchani

0
1934

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imepitisha kanuni za kuanzisha mabucha ya nyamapori, na pia imerekebisha kanuni za uanzishaji bustani, mashamba, na ranchi za wanyamapori.

Hayo yamesemwa leo Jumapili (Februari 9, 2020) na Waziri Hamis Kigwangalla kupitia ukurasa wake wa Twitter ambapo amewataka Watanzania kuchangamkia fursa hizo za kuichumi za kuuza nyama za wanyamapori kihalali pamoja na kufungua bustani za maonesho ya wanyamapori.

Kigwangalla amesema kuwa kupitia ridhaa iliyotolewa na Rais John Magufuli sasa mwananchi mwenye hamu na nyamapori anaweza kuipata kihalali.

“Tuliahidi kuanzisha mabucha ya nyamapori, tumetekeleza. Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dr. John Pombe Magufuli kwa kutoa ridhaa yake tuweze kufanya hivi. Sasa ukiwa na hamu ya nyamapori utaweza kuipata kihalali. Wajasiriamali hii nayo ni fursa mpya, changamkieni,” ameandika Kigwangalla.

Ili kuwawezesha wananchi kuwa na mashamba, bustani na ranchi za wanyamapori, serikali imeshusha bei za kununuliwa wanyamapori wa mbegu, pia uuzwaji utafanywa kupitia fedha ya Tanzania na si dola ya Marekani kama ilivyokuwa awali.

“Tumeshusha bei za kununulia wanyamapori wa mbegu kwa mtu anayetaka kuanzisha bustani, shamba ama ranchi ya wanyamapori. Zamani waliuzwa kwa dola za kimarekani kama zile za uwindaji wa kitalii, sasa tunauza kwa shilingi ya kitanzania kama zile za uwindaji wa wenyeji.”