Waziri Mkuu atia neno Samatta kusajiliwa Uingereza

0
518

Wakati mamilioni ya Watanzania wakiendelea kufurahia hatua aliyopiga nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mbwana Samatta baada ya kusajiliwa na klabu ya Aston Villa na kuanza kucheza soka nchini Uingereza, serikali imempongeza nyota huyo kwa kuweka historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kusakata kabumbu katika Ligi Kuu ya England.

Pongezi hizo zimetolewa leo bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitoa hoja ya kuahirisha Bunge ambapo amesema kuwa serikali inamtakia kila la heri katika ligi hiyo ambayo ni moja ya ligi ngumu zaidi duniani.

“Napenda nitumie nafasi hii kumpongeza mchezaji wetu Mbwana Samatta kwa kuweka historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kusajiliwa na kucheza Ligi Kuu ya England katika klabu ya Aston Villa, tunamtakia kila la heri,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha, ametoa wito kwa wachezaji wa mpira wa miguu hapa nchini kujifunza kupitia mafaniko ya Samatta kwa kuongeza bidii, nidhamu na kiu ya mafanikio kama ambavyo nyota huyo amefanikiwa.

Pia amezipongeza timu za taifa za wanawake chini ya umri wa miaka 20 na 17 kwa kuendelea kufanya vyema kuelekea kufuzu kushiriki kombe la dunia mwaka 2022.