Laini za simu milioni 12 hazijasajiliwa kwa alama za vidole

0
347
Kusajili laini kwa alama za vidole

Wakati baadhi ya wananchi wakiendelea na zoezi la kusajili laini zao za simu kwa alama za vidole, hadi Februari Pili mwaka huu kulikuwa na jumla ya laini milioni 43.9 nchini ambapo laini milioni 31.4 sawa na asilimia 71.6 tayari zimesajiliwa, ikimaanisha laini milioni 12.5 bado hazijasajili.

Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitoa hoja ya kuahirisha Bunge jijini Dodoma ambapo amesema zoezi la kusajili laini ni endelevu hivyo wananchi wote ambao laini zao zimefungwa kwa sababu hazikusajiliwa wakasajili.

Katika hoja yake ameeleza kuwa zoezi la kufunga laini ambazo hazijasajiliwa ni endelevu na ametoa wito kwa wananchi mara wapatapo namba au kitambulisho cha uraia waende kwa wakala au maduka husika kulingana na mitandao wanayotumia wakasajili ili kuepuka usumbufu wa kusitishiwa huduma za mawasiliano.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kusogeza huduma ya utoaji wa namba na vitambulisho kwenye vijiji ambavyo wananchi husika wanatoka.

“Ninatoa wito kwa NIDA kusogeza huduma za kutoa namba za vitambulisho karibu na wananchi mpaka kwenye ngazi za vijiji kadiri inavyowezekana. Lengo ni kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kupata namba za vitambulisho kwa ajili ya kuwawezesha kusajili laini zao za simu na vile vile kupata vitambulisho vya Taifa kwa ajili ya matumizi mengine muhimu,” ameeleza Waziri Mkuu.

Mkutano wa 18 wa Bunge la 11 uliomalizika leo, ulianza Januari 28 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine ulihusisha makabidhiano ya majoho kwa Maspika wastaafu, vipindi vya maswali na majibu kwa serikali, kuwasilishwa miswada ya serikali na kuwasilishwa kwa taarifa za Kamati za Bunge.